MAWASILIANO YA BLOG

KWA MAONI NA USHAURI WASILIANA NA OFISI YA HABARI NA MAWASILIANO KWA SIMU NAMBA 0764 143 977 AU E-MAIL: habarigeita@gmail.com

Friday 19 December 2014

KIWANGO CHA UFAULU MTIHANI WA DARASA LA SABA 2014 MKOA WA GEITA CHAONGEZEKA, WADAU WA ELIMU WATAKIWA KUONGEZA BIDII ZAIDI

Katibu Tawala Mkoa wa Geita Charles Pallangyo akifungua Kikao cha kutangaza matokeo na uteuzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Kwanza Mwaka 2015 Mkoa wa Geita. Mkoa wa Geita umefanikiwa kuongeza kiwango cha ufalu kwa mwaka huu kwa kufikia asilimia 63% kutoka asilimia 52% ya mwaka 2013.Akifungua Kikao hicho Ndugu Charles Pallangyo aliwaeleza wajumbe kuwa Mwaka 2014 Mkoa wa Geita ulikuwa na watahiniwa 28,473 wavulana wakiwa 13,934 na wasichana 14,539 waliosajiliwa na kufanya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi.Watahiniwa waliofanya mtihani ni 27,867 sawa na  98% ya wanafunzi 28,473 waliosajiliwa kufanya Mtihani.Aidha, Katibu Tawala alieleza kuwa wastani wa 63% ya Mkoa inadhihirisha kuwa sehemu kubwa ya watahiniwa ambao ni 10,294 walipata daraja la D na E ambayo ni chini ya alama 100 ya ufaulu.Watahiniwa 13,221 walifaulu kwa daraja C, 3,907 kwa daraja B na 432 daraja la A. Hali hiyo inaonesha kuwa ubora wa taaluma ya watahiniwa katika Mkoa upo chini. Hali inaashiria kwamba usimamizi na ufuatiliaji wa ufundishaji na ujifunzaji shuleni haukuwa wa kutosha.Kutokana na hali hii Katibu Tawala wa Mkoa ameagiza kuwa suala la ufuatiliaji wenye malengo ngazi ya shule liimarishwe na viongozi wa elimu wa Halmashauri zote kwa gharama yoyote.Aidha viongozi wote ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji wanapaswa kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha walimu wanafundisha ipasavyo na wanafunzi wanahudhuria shuleni siku zote za masomo, Wakurugenzi wa Halmashauri washirikiane na wakaguzi wa shule pale wanapokosa nyenzo za utekelezaji wa malengo na kutekeleza ushauri wa wakaguzi wa shule. Kwa Mkoa wa Geita Wanafunzi wote 17,560 waliofaulu mtihani wamepata nafasi ya kuingia kidato cha kwanza mwaka 2015 kwa kuanzia ufaulu wa asilimia 100. katika idadi hiyo wavulana ni 9,543 na wasichana 8,017.



Afisa Elimu Mkoa wa Geita Bi. Ephrasia Buchuma akitoa taarifa ya Elimu Mkoa wa Geita kwa wajumbe wa kamati ya Kutangaza matokeo na kutangaza uteuzi wa wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza mwaka 2015 Mkoa wa Geita. Katika taarifa hiyo Afisa Elimu alieleza kuwa hali ya ufaulu katika Mkoa hairidhishi sana japo kiwango cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia 11%  kutoka 52% mwaka 2013 hadi 63%  mwaka 2014. Hata hivyo, Mkoa wa Geita haukufikia lengo lake la 71% katika Mwaka huu hivyo aliwataka wadau wa elimu katika Mkoa kuongeza nguvu na bidii ili kuhakikisha kuwa Mkoa unapiga hatua zaidi katika masuala ya Elimu na kuongeza kiwango cha ufaulu. Aidha, Bi. Buchuma alitaja sababu za kutofanya vizuri kuwa ni mazingira magumu ya kazi kwa walimu, usimamizi duni wa elimu ngazi za halmashauri pamoja na utoro wa walimu, wanafunzi na kutozingatiwa kwa ratiba ya masomo kwa siku katika shule.


Wajumbe wa kamati ya uteuzi wa wanafunzi na utangazaji wa matokeo ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2015 wakifuatilia kwa makini wakati wa kikao hicho ambacho kimefanyika shule ya Sekondari Nyankumbu Halmashauri ya Mji Geita.


Mkuu wa Wilaya ya Geita Manzie Mangochie akizungumza na wajumbe wa kamati ya kutangaza matokeo Mkoa wa Geita kabla ya kumkaribisha Katibu Tawala wa Mkoa ili afungue kikao hicho cha kutangaza matokeo na uteuzi wawanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza mwaka 2015 Mkoa wa Geita.

Wajumbe wa Kamati ya uteuzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2015 Mkoa wa Geita wakiwa katika kikao cha kutangaza uteuzi wa wanafunzi na kutangaza matokeo darasa la saba Mkoa wa Geita kilichofanyika tarehe 19/12/2014 katika ukumbi wa shule ya Sekondari ya wasichana Nyankumbu.

Wednesday 3 December 2014

MAADHIMISHO YA WIKI YA UKIMWI DUNIANI MKOA WA GEITA YAFANYIKA KIJIJI CHA MGUSU WANANCHI WATAKIWA KUTUMIA NJIA NA HUDUMA ZILIZOPO KUPUNGUZA UGONJWA WA UKIMWI




Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Geita Fatma Mwassa akitoa msaada wa Mashuka,Daftari, kalamu,Sabuni na Ndoo kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi wilaya ya Geita ambao wamepatwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI wakati wa maadhimisho ya wiki ya UKIMWI Duniani ambapo katika Mkoa wa Geita maadhimisho hayo yamefanyika katika kijiji cha Mgusu wilayani Geita. Eneo hili la Mgusu ni eneo ambalo linamuingiliano mkubwa wa watu ambao wanajihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini aina ya dhahabu. Katika Maadhimisho hayo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alitoa wito kwa Viongozi na wananchi wote wa Mkoa wa Geita kuzitumia huduma zilizopo za kupambana na UKIMWI kikamilifu iliwafahamu afya zao na waweze kupata huduma na matibabu iwapo mtu atakuwa ameambukizwa virusi vya UKIMWI. Aidha, alisisitiza kuwa kila mwananchi ambaye amebainika kuambukizwa VVU,pale anapostahili kuanza kutumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI hana budi kuanza kutumia dawa hizo mara moja na kwa wakati kwakuwa mafanikio ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI yanategemea sana ufuasi wa matumizi sahihi ya dawa maisha yote. Vilevile aliitaka jamii kuwatia moyo wagonjwa walioanza kutumia dawa waendelee kuzitumia, pia jamii iwapatie lishe bora pamoja na ushauri wa kiroho.Kutokana na tafiti zilizofanyika hapa nchini kiwango cha maambukizi ya virusi vya UKIMWI Mkoa wa Geita ni 4.7% ukilinganisha na ya kitaifa ambayo ni 5.1%.Katika miaka miwili mfulilizo yaani 2013/2014 kati ya watu 148,753 walichukuliwa damu ambapo kati ya hao wanaume  walikuwa 83,302 na wanawake 65,451 hata hivyo wanaume 37,486 na wanawake 39,998 walikutwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI.

Tuesday 2 December 2014



Vikundi vya Kwaya kutoka Mgusu vikitumbuiza  katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani.

Viongozi mbalimbali wa serikali na taasisi binafsi wakiwa wamejitokeza katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo katika Mkoa wa Geita ilifanyika kijiji cha Mgusu wilayani Geita.


Wananchi wa Kijiji cha Mgusu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mgusu wakiwa wamejitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniania ambapo katika Mkoa wa Geita Maadhimisho hayo yamefanyika Kijiji cha Mgusu Kata ya Mtakuja Wilaya ya Geita.