Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Geita Fatma Mwassa akitoa msaada wa Mashuka,Daftari, kalamu,Sabuni na Ndoo kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi wilaya ya Geita ambao wamepatwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI wakati wa maadhimisho ya wiki ya UKIMWI Duniani ambapo katika Mkoa wa Geita maadhimisho hayo yamefanyika katika kijiji cha Mgusu wilayani Geita. Eneo hili la Mgusu ni eneo ambalo linamuingiliano mkubwa wa watu ambao wanajihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini aina ya dhahabu. Katika Maadhimisho hayo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alitoa wito kwa Viongozi na wananchi wote wa Mkoa wa Geita kuzitumia huduma zilizopo za kupambana na UKIMWI kikamilifu iliwafahamu afya zao na waweze kupata huduma na matibabu iwapo mtu atakuwa ameambukizwa virusi vya UKIMWI. Aidha, alisisitiza kuwa kila mwananchi ambaye amebainika kuambukizwa VVU,pale anapostahili kuanza kutumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI hana budi kuanza kutumia dawa hizo mara moja na kwa wakati kwakuwa mafanikio ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI yanategemea sana ufuasi wa matumizi sahihi ya dawa maisha yote. Vilevile aliitaka jamii kuwatia moyo wagonjwa walioanza kutumia dawa waendelee kuzitumia, pia jamii iwapatie lishe bora pamoja na ushauri wa kiroho.Kutokana na tafiti zilizofanyika hapa nchini kiwango cha maambukizi ya virusi vya UKIMWI Mkoa wa Geita ni 4.7% ukilinganisha na ya kitaifa ambayo ni 5.1%.Katika miaka miwili mfulilizo yaani 2013/2014 kati ya watu 148,753 walichukuliwa damu ambapo kati ya hao wanaume walikuwa 83,302 na wanawake 65,451 hata hivyo wanaume 37,486 na wanawake 39,998 walikutwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI. |