MAWASILIANO YA BLOG

KWA MAONI NA USHAURI WASILIANA NA OFISI YA HABARI NA MAWASILIANO KWA SIMU NAMBA 0764 143 977 AU E-MAIL: habarigeita@gmail.com

Friday 19 December 2014

KIWANGO CHA UFAULU MTIHANI WA DARASA LA SABA 2014 MKOA WA GEITA CHAONGEZEKA, WADAU WA ELIMU WATAKIWA KUONGEZA BIDII ZAIDI

Katibu Tawala Mkoa wa Geita Charles Pallangyo akifungua Kikao cha kutangaza matokeo na uteuzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Kwanza Mwaka 2015 Mkoa wa Geita. Mkoa wa Geita umefanikiwa kuongeza kiwango cha ufalu kwa mwaka huu kwa kufikia asilimia 63% kutoka asilimia 52% ya mwaka 2013.Akifungua Kikao hicho Ndugu Charles Pallangyo aliwaeleza wajumbe kuwa Mwaka 2014 Mkoa wa Geita ulikuwa na watahiniwa 28,473 wavulana wakiwa 13,934 na wasichana 14,539 waliosajiliwa na kufanya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi.Watahiniwa waliofanya mtihani ni 27,867 sawa na  98% ya wanafunzi 28,473 waliosajiliwa kufanya Mtihani.Aidha, Katibu Tawala alieleza kuwa wastani wa 63% ya Mkoa inadhihirisha kuwa sehemu kubwa ya watahiniwa ambao ni 10,294 walipata daraja la D na E ambayo ni chini ya alama 100 ya ufaulu.Watahiniwa 13,221 walifaulu kwa daraja C, 3,907 kwa daraja B na 432 daraja la A. Hali hiyo inaonesha kuwa ubora wa taaluma ya watahiniwa katika Mkoa upo chini. Hali inaashiria kwamba usimamizi na ufuatiliaji wa ufundishaji na ujifunzaji shuleni haukuwa wa kutosha.Kutokana na hali hii Katibu Tawala wa Mkoa ameagiza kuwa suala la ufuatiliaji wenye malengo ngazi ya shule liimarishwe na viongozi wa elimu wa Halmashauri zote kwa gharama yoyote.Aidha viongozi wote ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji wanapaswa kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha walimu wanafundisha ipasavyo na wanafunzi wanahudhuria shuleni siku zote za masomo, Wakurugenzi wa Halmashauri washirikiane na wakaguzi wa shule pale wanapokosa nyenzo za utekelezaji wa malengo na kutekeleza ushauri wa wakaguzi wa shule. Kwa Mkoa wa Geita Wanafunzi wote 17,560 waliofaulu mtihani wamepata nafasi ya kuingia kidato cha kwanza mwaka 2015 kwa kuanzia ufaulu wa asilimia 100. katika idadi hiyo wavulana ni 9,543 na wasichana 8,017.