MAWASILIANO YA BLOG

KWA MAONI NA USHAURI WASILIANA NA OFISI YA HABARI NA MAWASILIANO KWA SIMU NAMBA 0764 143 977 AU E-MAIL: habarigeita@gmail.com

Friday 19 December 2014

KIWANGO CHA UFAULU MTIHANI WA DARASA LA SABA 2014 MKOA WA GEITA CHAONGEZEKA, WADAU WA ELIMU WATAKIWA KUONGEZA BIDII ZAIDI

Katibu Tawala Mkoa wa Geita Charles Pallangyo akifungua Kikao cha kutangaza matokeo na uteuzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Kwanza Mwaka 2015 Mkoa wa Geita. Mkoa wa Geita umefanikiwa kuongeza kiwango cha ufalu kwa mwaka huu kwa kufikia asilimia 63% kutoka asilimia 52% ya mwaka 2013.Akifungua Kikao hicho Ndugu Charles Pallangyo aliwaeleza wajumbe kuwa Mwaka 2014 Mkoa wa Geita ulikuwa na watahiniwa 28,473 wavulana wakiwa 13,934 na wasichana 14,539 waliosajiliwa na kufanya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi.Watahiniwa waliofanya mtihani ni 27,867 sawa na  98% ya wanafunzi 28,473 waliosajiliwa kufanya Mtihani.Aidha, Katibu Tawala alieleza kuwa wastani wa 63% ya Mkoa inadhihirisha kuwa sehemu kubwa ya watahiniwa ambao ni 10,294 walipata daraja la D na E ambayo ni chini ya alama 100 ya ufaulu.Watahiniwa 13,221 walifaulu kwa daraja C, 3,907 kwa daraja B na 432 daraja la A. Hali hiyo inaonesha kuwa ubora wa taaluma ya watahiniwa katika Mkoa upo chini. Hali inaashiria kwamba usimamizi na ufuatiliaji wa ufundishaji na ujifunzaji shuleni haukuwa wa kutosha.Kutokana na hali hii Katibu Tawala wa Mkoa ameagiza kuwa suala la ufuatiliaji wenye malengo ngazi ya shule liimarishwe na viongozi wa elimu wa Halmashauri zote kwa gharama yoyote.Aidha viongozi wote ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji wanapaswa kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha walimu wanafundisha ipasavyo na wanafunzi wanahudhuria shuleni siku zote za masomo, Wakurugenzi wa Halmashauri washirikiane na wakaguzi wa shule pale wanapokosa nyenzo za utekelezaji wa malengo na kutekeleza ushauri wa wakaguzi wa shule. Kwa Mkoa wa Geita Wanafunzi wote 17,560 waliofaulu mtihani wamepata nafasi ya kuingia kidato cha kwanza mwaka 2015 kwa kuanzia ufaulu wa asilimia 100. katika idadi hiyo wavulana ni 9,543 na wasichana 8,017.



Afisa Elimu Mkoa wa Geita Bi. Ephrasia Buchuma akitoa taarifa ya Elimu Mkoa wa Geita kwa wajumbe wa kamati ya Kutangaza matokeo na kutangaza uteuzi wa wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza mwaka 2015 Mkoa wa Geita. Katika taarifa hiyo Afisa Elimu alieleza kuwa hali ya ufaulu katika Mkoa hairidhishi sana japo kiwango cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia 11%  kutoka 52% mwaka 2013 hadi 63%  mwaka 2014. Hata hivyo, Mkoa wa Geita haukufikia lengo lake la 71% katika Mwaka huu hivyo aliwataka wadau wa elimu katika Mkoa kuongeza nguvu na bidii ili kuhakikisha kuwa Mkoa unapiga hatua zaidi katika masuala ya Elimu na kuongeza kiwango cha ufaulu. Aidha, Bi. Buchuma alitaja sababu za kutofanya vizuri kuwa ni mazingira magumu ya kazi kwa walimu, usimamizi duni wa elimu ngazi za halmashauri pamoja na utoro wa walimu, wanafunzi na kutozingatiwa kwa ratiba ya masomo kwa siku katika shule.


Wajumbe wa kamati ya uteuzi wa wanafunzi na utangazaji wa matokeo ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2015 wakifuatilia kwa makini wakati wa kikao hicho ambacho kimefanyika shule ya Sekondari Nyankumbu Halmashauri ya Mji Geita.


Mkuu wa Wilaya ya Geita Manzie Mangochie akizungumza na wajumbe wa kamati ya kutangaza matokeo Mkoa wa Geita kabla ya kumkaribisha Katibu Tawala wa Mkoa ili afungue kikao hicho cha kutangaza matokeo na uteuzi wawanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza mwaka 2015 Mkoa wa Geita.

Wajumbe wa Kamati ya uteuzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2015 Mkoa wa Geita wakiwa katika kikao cha kutangaza uteuzi wa wanafunzi na kutangaza matokeo darasa la saba Mkoa wa Geita kilichofanyika tarehe 19/12/2014 katika ukumbi wa shule ya Sekondari ya wasichana Nyankumbu.

Wednesday 3 December 2014

MAADHIMISHO YA WIKI YA UKIMWI DUNIANI MKOA WA GEITA YAFANYIKA KIJIJI CHA MGUSU WANANCHI WATAKIWA KUTUMIA NJIA NA HUDUMA ZILIZOPO KUPUNGUZA UGONJWA WA UKIMWI




Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Geita Fatma Mwassa akitoa msaada wa Mashuka,Daftari, kalamu,Sabuni na Ndoo kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi wilaya ya Geita ambao wamepatwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI wakati wa maadhimisho ya wiki ya UKIMWI Duniani ambapo katika Mkoa wa Geita maadhimisho hayo yamefanyika katika kijiji cha Mgusu wilayani Geita. Eneo hili la Mgusu ni eneo ambalo linamuingiliano mkubwa wa watu ambao wanajihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini aina ya dhahabu. Katika Maadhimisho hayo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alitoa wito kwa Viongozi na wananchi wote wa Mkoa wa Geita kuzitumia huduma zilizopo za kupambana na UKIMWI kikamilifu iliwafahamu afya zao na waweze kupata huduma na matibabu iwapo mtu atakuwa ameambukizwa virusi vya UKIMWI. Aidha, alisisitiza kuwa kila mwananchi ambaye amebainika kuambukizwa VVU,pale anapostahili kuanza kutumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI hana budi kuanza kutumia dawa hizo mara moja na kwa wakati kwakuwa mafanikio ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI yanategemea sana ufuasi wa matumizi sahihi ya dawa maisha yote. Vilevile aliitaka jamii kuwatia moyo wagonjwa walioanza kutumia dawa waendelee kuzitumia, pia jamii iwapatie lishe bora pamoja na ushauri wa kiroho.Kutokana na tafiti zilizofanyika hapa nchini kiwango cha maambukizi ya virusi vya UKIMWI Mkoa wa Geita ni 4.7% ukilinganisha na ya kitaifa ambayo ni 5.1%.Katika miaka miwili mfulilizo yaani 2013/2014 kati ya watu 148,753 walichukuliwa damu ambapo kati ya hao wanaume  walikuwa 83,302 na wanawake 65,451 hata hivyo wanaume 37,486 na wanawake 39,998 walikutwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI.

Tuesday 2 December 2014



Vikundi vya Kwaya kutoka Mgusu vikitumbuiza  katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani.

Viongozi mbalimbali wa serikali na taasisi binafsi wakiwa wamejitokeza katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo katika Mkoa wa Geita ilifanyika kijiji cha Mgusu wilayani Geita.


Wananchi wa Kijiji cha Mgusu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mgusu wakiwa wamejitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniania ambapo katika Mkoa wa Geita Maadhimisho hayo yamefanyika Kijiji cha Mgusu Kata ya Mtakuja Wilaya ya Geita.

Tuesday 25 November 2014

KATIBU TAWALA MPYA MKOA WA GEITA AKABIDHIWA RASMI OFISI AWATAKA WATUMISHI KUONYESHA USHIRIKIANO KATIKA UTENDAJI KAZI


Katibu Tawala Mkoa wa Geita ndugu Charles Pallangyo wakwanza kulia walio simama akikabidhiwa rasmi nyaraka za Ofisi na aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Geita Severine Kahitwa ambaye amehamia Mkoa wa Kilimanjaro.
Aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Geita  Ndugu Severine Kahitwa akiweka saini katika nyaraka mbalimbali za serikali na kumkabidhi rasmi nyaraka hizo Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Geita Ndugu Charles Pallangyo.

Katibu Tawala Mpya Mkoa wa Geita Ndugu Charles Pallangyo akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Geita na Taasisi nyingine za Umma na mashirika ambao walihudhuria Sherehe za Makabidhiano ya Ofisi kati yake na aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa huu Ndugu Severine Kahitwa. Katika makabidhiano hayo ndugu Pallangyo aliwataka watumishi kuonyesha ushirikiano na kufanya kazi kwa bidii katika majukumu yao ya kila siku huku akiwaagiza wakuu wa idara zote kuhakikisha kuwa wanafanya vikao na watumishi kila mwezi na muhtasari wa vikao hivyo unawasilishwa kwake mapema iwezekanavyo.Aidha aliwaomba wadau wote wa maendeleo kutoa ushirikiano katika masuala ya maendeleo ya Mkoa huu pale watakapohitajika kufanya hivyo.

Aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa Mkoa wa Geita ambaye sasa ni Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Severine Kahitwa akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita wakati wa sherehe za kukabidhi Ofisi kwa Katibu Tawala Mpya wa Mkoa wa Geita.Katika sherehe hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita Ndugu Kahitwa aliwashukuru watumishi kwa ushirikiano waliompa wakati wa utendaji kazi wake katika Mkoa wa Geita na aliwataka kuendeleza mema hayo kwa kufanya kazi kwa bidii na uhadilifu wa hali ya juu kwa lengo la kuleta maendeleo katika Mkoa  wa Geita.

Baadhi ya wageni waalikwa na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita,Taasisi za Umma na Mashirika wakiwa katika ukumbi wa Mikutato Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita wakifuatilia kwa karibu shughuli ya Makabidhiano ya Ofisi baina ya Katibu Tawala wa Mkoa anayehama ndugu Severine Kahitwa (Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro) na Katibu Tawala Mpya wa Mkoa wa Geita Ndugu Charles Pallangyo.

Makatibu Tawala wa Mikoa ya Geita na Kilimanjaro wapili na watatu kwa waliokaa kutoka kulia wakiwa katika picha ya pamoja Wakuu wa Idara Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita wakati wa sherehe za makabidhiano ya Ofisi baina ya ndugu Severine Kahitwa ambaye alikuwa Katibu Tawala Mkoa wa Geita ambaye anahamia Mkoa wa Kilimanjaro na ndugu Charles Pallangyo ambaye ndiye Katibu Tawala Mpya wa Mkoa wa Geita.

Makatibu Tawala wa Mikoa ya Geita na Kilimanjaro wapili na watatu (waliokaa) kutoka kulia wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Idara ya Utawala na rasilimali watu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. katika sherehe za makabidhiano ya Ofisi baina ya viongozi hao.Wakwanza kushoto waliokaa ni Mkuu wa Idara ya Utawala na rasilimali watu Bw: Samsoni Mashalla na wakwanza kulia ni Afisa Utumishi Mwandamizi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita Bw: Magange .H. Mwita.

Monday 24 November 2014

Makatibu Tawala wa Mikoa ya Geita na Kilimanjaro wapili na watatu  walio kaa kutoka kulia wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa idara ya Elimu ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita wakati wa sherehe fupi ya makabidhiano ya Ofisi baina ya viongozi hao.Wengine walio kaa wakwanza kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu ndugu Samson Mashalla na wakwanza kulia ni Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Elimu Bi Ephrasia Buchuma.

Makatibu Tawala wa Mikoa ya Geita na Kilimanjaro wapili na watatu walio kaa kutoka kulia wakiwa katika Picha ya pamoja na viongozi na wawakilishi wa Taasisi za Umma na binafsi wakati wa sherehe fupi za makabidhiano ya Ofisi baina ya aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita ndugu Severine Kahitwa ambaye amehamia Mkoa wa Kilimanjaro na Ndugu Charles Pallangyo Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Geita.

Wednesday 12 November 2014

MKUTANO WA TISA WA WADAU WA SEKTA NDOGO YA PAMBA WAFANYIKA MKOANI GEITA

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita Amani Mwenegoha akihutubia katika Mkutano wa wadau wa Sekta ndogo ya Pamba Mkoa wa Geita.Katika Mkutano huo ambao Mhe Amani alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa  Geita Mhe.Fatma Mwassa aliwapongeza kwa dhati viongozi wa Bodi ya Pamba kwa kushirikiana ta Tanzania Gastby Trust kwa kuendelea kuwezesha utaratibu wa wadau wa Pamba kukutana kila baada ya miezi mitatu uamuzi ambao utawanufaisha wakulima na Wafanyabiashara wa zao la Pamba Mkoa wa Geita.Mkutano huo ulikusudia kujadili kwa kina mkakati wa utekelezaji wa kilimo mkataba katika msimu 2014/2015, Mkakati wa kila halmashauri katika kuongeza uzalishaji wa Pamba kutoka kilo 400 kufikia kilo 800 kwa ekari.

Katibu Tawala msaidizi Idara ya Uchumi na uzalishaji ndugu Emili Kasagala akiwaongoza wajumbe wa Mkutano katika agenda za Mkutano wa wadau wa Sekta ndogo ya Pamba Mkoa wa Geita.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba kanda ya Ziwa ndugu kalidushi Buruma akichangia mada kuhusu kilimo cha mkataba cha Pamba wakati wa Mkutano wa tisa wa Sekta ndogo ya Pamba Mkoa wa Geita.

Mwakilishi wa Kampuni ya Tanzania Gast Trust (TGT) Dr. Sililima akichangia mada kuhusu kilimo cha Pamba cha Mkataba wakati wa Mkutano wa tisa wa wadau wa Sekta ndogo ya Pamba Mkoa wa Geita.

Mwakilishi wa Kampuni ya Quton ndugu Benedicto Massele akitoa ufafanuzi kuhusu Mbegu za Pamba za Quton (mbegu zisizo na manyoya) wakati wa Mkutano wa tisa wa Sekta ndogo ya Pamba Mkoa wa Geita.

Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale ndugu Gudala Kija akitoa maelezo kuhusu kilimo cha Pamba wakati wa Mkutano wa wadau wa Sekta ndogo ya Pamba Mkoa wa Geita.

Mkulima wa zao la Pamba Wilaya ya Nyang'hwale ndugu Masoud Mtore akichangia mada wakati wa Mkutano  wa tisa wa wadau wa Sekta ndogo ya pamba Mkoa wa Geita.


Wadau wa Sekta ndogo ya Pamba Mkoa wa Geita wakiwa katika ukumbi wa Mkutano wakati wa mkutano wa tisa wa sekta hiyo hivi karibuni Mkoani Geita.


Wadau wa Sekta ndogo ya Pamba Mkoa wa Geita wakifuatilia kwa makini Mkutano wa tisa wa sekta hiyo uliofanyika hivi karibuni Mkoani Geita.

Tuesday 21 October 2014

MKOA WA GEITA WAZINDUA CHANJO YA SURUA-RUBELLA KWA WATOTO WA MIEZI 9 HADI CHINI YA MIAKA 15

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Geita Magalula Saidi Magalula akizindua chanjo ya Surua-Rubella kwa kumpa mtoto matone na dawa za minyoo huku akishuhudiwa na viongozi wengine wa serikali waliohudhulia ulinduzi huo uliofanyika katika kituo cha Afya Nyankumbu nje kidogo ya Mji wa Geita.Watoto 923,000 katika Mkoa wa Geita wanategemea kupata chanzo hizo.


Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Geita Magalula Saidi akiwahutubia wananchi wakati wa Uzinduzi Chanjo ya Surua - Rubella ambao ulifanyika katika kituo cha Afya Nyankumbu Halmashauri ya Mji wa Geita. Mhe Mkuu wa Mkoa alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wazazi na wanajamii kuwa Chanjo ni haki ya kila mtoto na ni jukumu la kila mzazi au mlezi kuhakikisha kuwa watoto wanapata chanjo na huduma nyingine muhimu za afya kama matone ya vitamini A na dawa za minyoo.Aidha alitoa angalizo kwa wananchi kuwa kuna kazi kubwa ya kuwaelimisha kuhusu kampeni ya chanjo ya Surua-Rubella ambayo inatolewa sanjali na huduma nyingine hivyo aliwataka wasaidiane na serikali kupeleka taarifa sahihi kwa wenzao ili kuepusha upotoshaji. ''Kila mmoja wetu anawajibu wa kuelimisha na kuhamasisha mwenzake ili tuweze kujitokeza kwa wingi wakati wa kampeni kwa kuwaleta watoto wote kupata chanjo kwa faida ya Afya zao ,Mkoa na Taifa''. Aliwataka wananchi kuwapeleka watoto katika vituo vya kutolea chanjo ili wakingwe dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo na kuboresha maisha na afya zao.

Monday 20 October 2014

Mkuu wa Wilaya ya Geita Manzie Mangochie akizungumza na wananchi wa Nyankumbu wakati wa uzinduzi wa Chanjo ya Surua - Rubella Mkoani Geita ambao ulifanyika katika kituo cha Afya Nyankumbu Halmashauri ya Mji Geita.


Wasanii wa kikundi cha ngoma za asili cha Bakomyalumi kutoka halmashauri ya Mji wa Geita wakitumbuiza wakati wa uzinduzi wa Chanjo ya Surua - Rubella Mkoani Geita.

Mkuu wa Mkoa wa Geita mhe Magalula Saidi   wapili kutoka kulia akipata maelezo kutoka kwa mhudumu wa Afya namna shughuli za utoaji chanzo zinavyoendelea wakati wa uzinduzi wa chanjo hizo Mkoani Geita.Wakwanza kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa Geita Dr.Kisala na watatu ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita ndugu Severine Kahitwa.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.Magalula Said Magalula wapili kutoka kulia kwa walio simama akijionea namna shughuli za utoaji chanjo, matone na dawa za minyoo  kwa watoto wa miezi 9 hadi chini ya miaka 15 zinavyoendelea wakati wa uzinduzi wa chanjo ya Surua- Rubella Mkoani Geita,wakwanza kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dr.Joseph Kisala.

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Geita Magalula Saidi Magalula akizungumza na akina mama waliojitokeza katika uzinduzi wa Chanjo ya Surua-Rubella ambao katika Mkoa wa Geita Uzinduzi huo ulifanyika katika Kituo cha Afya Nyankumbu Halmashauri ya Mji Geita.