MAWASILIANO YA BLOG

KWA MAONI NA USHAURI WASILIANA NA OFISI YA HABARI NA MAWASILIANO KWA SIMU NAMBA 0764 143 977 AU E-MAIL: habarigeita@gmail.com

Thursday 30 April 2015

FAHAMU YALIYOJILI KATIKA KIKAO CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI MKOA WA GEITA LILILOFANYIKA TAREHE 29/04/2015

Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi Mkoa wa Geita Ndugu Charles Pallangyo (katikati kwa waliokaa meza ya mbele) akiwahutubia wajumbe wa baraza hilo wakati wa kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Geita ambapo aliwataka wajumbe hao kuhakikisha kuwa wanaelimisha wafanyakazi wengine katika maeneo yao kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za Utumishi wa Umma katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Aidha Ndugu Charles Pallangyo ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita aliwataka wafanyakazi wote wa Mkoa wa Geita kufanya kazi kwa kuzingatia utawala bora na kujiepusha na vitendo vyote vinavyoashiria rushwa na kutimiza wajibu ili wananchi waendelee kuiamini serikali. Vilevile aligusia suala la UKIMWI katika mazingira ya kazi ambapo aliwataka wafanyakazi wote kujilinda na kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo hatari ambapo aliwataka kuhakikisha wanajenga tabia ya kupima afya mara kwa mara na wale wanaokutwa na maambukizi wajitokeze wapate huduma kwasababu serikali inawahudumia watumishi wa namna hiyo kwa kuwapatia fedha ya matibabu pamoja na lishe na kwa wale ambao hawana maambukizi walitakiwa kujilinda na kijiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha wao kuambukizwa ugonjwa huo hatari kwa taifa na dunia.Aidha aliwataka wajumbe na wafanyakazi kuwa wavumilivu kwakuwa serikali inatambua kero zao na inazitafutia ufumbuzi kwa lengo la kuboresha maisha yao.

Katibu wa Chama cha wafanyakazi (TUGHE) Mkoa wa Geita  Bi. Ethel Kahuluda akizungumza na wajumbe wa baraza ambapo aliwaeleza namna wafanyakazi wanavyotakiwa kuwa wakati wa kutimiza majukumu yao ya kila siku na pia pale wanapozungumza na viongozi au waajiri wao. Alisema kuwa wafanyakazi wana kero nyingi zinazowakabili lakini ni vyema wakawa wavumilivu na watulivu wakati wa kudai haki zao za msingi napia wahakikishe kuwa pamoja na kudai haki hizo pia watimize wajibu wao ipasavyo wakati wa kuhudumia wananchi.

Katibu wa Baraza la wafanyakazi Mkoa wa Geita Bi. Sania Mwangakala akiwakaribisha wajumbe wa baraza hilo pamoja na Mwenyekiti wa Baraza Ndugu Charles Pallangyo ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita(katikati) pamoja na Katibu wa Chama cha wafanyakazi Mkoa wa Geita(TUGHE) Bi. Ethel Kahuluda wa kwanza kulia. Katika kikao hicho Bi. Sania aliwaeleza wajumbe kuwa madhumuni ya kikao hicho ni kujadili changamoto zinazowakabili wafanya kazi na kuzitafutia ufumbuzi.Hata hivyo katika kikao hicho kulifanyika uchaguzi wa katibu wa baraza hilo baada ya Bi. Sania kuwa na majukumu mengine ya kikazi hivyo nafasi yake kuchukuliwa na ndugu Magange Hamisi Mwita na naibu katibu kuwa ndugu Sara Mwangole wote kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Mratibu wa UKIMWI Mkoa wa Geita Dkt. Joseph Odero akiwasilisha mada kuhusu UKIMWI ambapo aliwataka wajumbe kuwahamasisha wafanyakazi kuwa na tabia ya kupima virus vya UKIMWI na pale watakapo jitambua kuwa wameathirika wajitokeze ili wapate huduma, pia kama hawajaambukizwa ni bora wakatumia njia za kujikinga na maradhi hayo au kuwa waaminifu au kujizuia kabisa.

Mjumbe wa baraza la wafanyakazi Mkoa wa Geita ndugu D.B Kayango ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Mipango Mkoa wa Geita akiwasilisha bajeti ya Mkoa wa Geita kwa Mwaka 2015/2016 mbele ya wajumbe wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Mjumbe wa baraza la wafanyakazi la Mkoa wa Geita Ndugu Mathayo Maselle akichangia Mada kuhusu UKIMWI iliyowasilishwa na Mratibu wa UKIMWI Mkoa Dkt. Joseph Odero wakati wa kikao.

Mganga Mkuu wa Mkoa Geita Dkt. Joseph Kisala akitoa ufafanuzi  kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi Mkoa wa Geita wakati wa kikao kilichofanyika tarehe 29/04/2015 kuhusu utaratibu wa malipo ya posho ya muda wa ziada wa kazi kwa madaktari na wauguzi wa hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Mkoa wa Geita wakifuatilia kwa karibu makaburasha wakati  wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa lengo la kujadili changamoto zinazowakabili wafanyakazi na kuzitafutia ufumbuzi.(Picha-Afisa Habari RS-GEITA)