Mkuu wa Mkoa wa Geita Mh. Magalula Said Magalula akifafanua kuhusu utekelezaji wa miradi ya barabara Mkoa wa Geita |
MKUU WA MKOA APONGEZA
UTEKELEZAJI WA MIRADI YA BARABARA MKOA WA GEITA
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.
Magalula Saidi Magalula amewapongeza viongozi na watu mbalimbali wote
waliohusika kwa namna yeyote ile katika usimamizi wa utekelezaji wa miradi yote
ya barabara inayotekelezwa ndani ya Mkoa wa Geita.
Mhe. Magalula aliyasema hayo
katika kikao maalum cha bodi ya ushauri ya barabara ya Mkoa (Road Board)
kilichofanyika Mjini Geita katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Wilaya
ya Geita na kuwashirikisha viongozi mbalimbali wa Wilaya,viongozi wa vyama vya
siasa na wataalam wa ujenzi wa barabara ambapo walielezwa kwamba Mkoa umepata
mafanikio katika utekelezaji wa miradi midogo na mikubwa ya barabara ambayo
inaendelea kutekelezwa kwa kiwango cha lami.
Katika kikao hicho Mhe.Mkuu wa
Mkoa alizitaka mamlaka za serikali za mitaa pamoja na Tanroads Mkoa wa Geita
ziendelee kuhakikisha kwamba shughuli za ujenzi na ukarabati wa barabara
zinatolewa kwa wakandarasi wenye vigezo vya uzoefu, uwezo, wataalam na mitambo
ya uhakika na pia kufuatilia na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo
ili kufikia kiwango sahihi na thamani ya fedha ionekane katika miradi husika.
Katika hatua nyingine Mhe.
Magalula alizitaka Halmashauri za Wilaya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi
kuhusu kutovamia hifadhi za barabara na pia kuweka mipaka ya barabara ili
kuepusha uharibifu wa barabara. Aidha, alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa
wananchi wenye tabia ya wizi wa alama za barabara na kupitisha mifugo katikati
ya barabara na kuacha mara moja tabia hizo kwani zinasababisha
hasara kubwa kwa serikali na kuziagiza
kamati za ulinzi na usalama,ulinzi shirikishi kuweka utaratibu mzuri wa kulinda
na kutunza barabara.
Mkoa wa Geita una mtandao wa
barabara zenye Kilometa 6,650.75 huku barabara za kiwango cha lami zikiwa ni
kilometa 485, changarawe ni kilometa 3,381.05 na barabara za udongo ni kilometa
2,784.70.
Miradi inayotekelezwa kwa kiwango
cha lami ni pamoja na ujenzi wa barabara ya “Round about” - Benki ya CRDB -
Hospitali ya Wilaya - Benki ya NMB na kuunga barabara kuu ( KM 1) kwa usimamizi
wa Tanroads kwa gharama ya Tshs 450 milioni imekamilika kwa asilimia 98.Ujenzi
wa barabara ya Nyankumbu-Nyanghwale (km 91) unaendelea kujengwa kwa KM 2 kutoka
Nyankumbu hadi Mkolani ujenzi umefikia asilimia 60 na itagharimu kiasi cha
million 750 mpaka kukamilisha kilometa 2 za lami ujenzi huo unasimamiwa na Tanroads. Aidha kuna ujenzi unaoendelea wa
barabara ya CRDB- Boman i- Magereza (km1) kwa kiwango cha lami ambao umefikia asilimia 24 ambao utagharimu
Tshs 438 milioni.
Miradi mikubwa ya ujenzi wa
barabara inayotekelezwa na serikali na kusimamiwa na Tanroads katika Mkoa wa
Geita ni pamoja na Bwanga- Biharamulo (KM 67) kwa gharama ya Tshs 55 bilioni na
Bwanga –Uyovu (KM 45) kwa gharama ya Tshs 43.3 bilioni miradi hii yote imefikia
asilimia nzuri na iliwekewa jiwe la msingi na Mhe. Rais wakati wa ziara yake
Mkoani Geita.
Na. Magesa Jumapili (Geita)