Mheshimiwa Fatma Mwassa Mkuu wa Mkoa wa Geita akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Igate wilaya ya Geita punde baada ya kufungua ghala la kuhifadhi matunda na mbogamboga la kijiji hicho ambalo limejengwa kwa msaada wa shirika lisilo la kiserikali ACCORD kwa ghalama ya Tshs milioni 53 kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa kata za Nzera ,Bugando, Katoma ambao ni maalufu kwa kilimo cha Nanasi kuhifadhi na kuuza matunda hayo katika ghala hilo. Katika hotuba yake Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliwataka wananchi hasa vijana kufanya kazi kwa bidii ili wajiletee maendeleo. Hata hivyo Mkuu wa Mkoa aliwaeleza wananchi kuwa serikali inafanya kila linalowezekana ili kuwatafutia wakulima wa zao la nanasi soko la ndani na nje ili kuwainua kiuchumi. Vilevile alisema kuwa serikali inatambua mchango wa zao la nanasi katika Mkoa wa Geita hivyo itaunda vikundi viwili vya mfano na kuviwezesha utaalamu, mbegu, mbolea na misaada mingine ili vianze kulima na kuzalisha nanasi kwa wingi na kuongeza kipato kwa vijana na jamii kwa jumla. Kijiji cha Igate kinalima jumla ya ekeri 769 ambazo uzalisha zaidi ya tani 27,600 kwa mwaka katika awamu tatu za mavuno ambapo kila awamu hutoa tani 9,228. Aidha katika kuhakikisha kuwa wananchi wanajiongezea kipato wamejiunga katika kikundi cha UWAMAMI ambacho mpaka sasa kina jumla ya wanachama 91 ambao wanatumia ekari 71 katika kilimo cha mbogamboga na ekari 283 katika kilimo cha nanasi. |