Mkuu
wa Mkoa wa Geita Mhe. Magalula Saidi amefanya ziara ya kikazi ya siku nne (4) wilaya ya
Nyang’hwale Mkoani Geita.
Akiwa katika
ziara hiyo Mhe. Mkuu wa wa Mkoa alikagua shughuli mbalimbali kubwa zaidi ikiwa
ni ukaguzi wa masuala ya elimu hasa suala la kuwapeleka wanafunzi waliofaulu
kuendelea na kidato cha kwanza shuleni katika wilaya hiyo ambapo alizitembelea
shule mbalimbali za sekondari ikiwa ni
pamoja Busolwa, Nyijundu, Kafita, Mwingiro,Nyang’hwale na Bukwimba Sekondari.
Aidha katika
ziara hiyo Mhe. Mkuu wa Mkoa alizitembelea shule za msingi mbalimbali kwa lengo
la kukagua suala la utengenezaji wa madawati na uandikishwaji wa wanafunzi
wanaoanza darasa la kwanza ambapo aliwataka wazazi wote kuwapeleka watoto wao
shuleni hivyo hivyo walivyo wakati taratibu za kutimiza mahitaji yao
zikifanyika wanafunzi wakiwa shuleni.
Katika hatua
nyingine Mhe. Magalula Saidi aliwataka viongozi wa kata na vijiji kuwachukulia
hatua kali za kisheria wazazi wote ambao hawajawapeleka watoto wao shule ikiwa
ni pamoja na kuwafikisha mahakamani .
Sambamba na
hilo Mhe. Mkuu wa Mkoa alifanya mikutano
ya hadhara katika maeneo yote aliyopita wakati wa ziara yake ambapo
alikemea vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na kuwauwa watu wasiokuwa na
hatia kwa kisingizio cha imani za kishirikina na hasira kali.
Ziara hiyo
imesaidia sana kuamsha ari ya wananchi kupenda kuwapeleka watoto shule na pia
kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
Na: Magesa Jumapili