WAKURUGENZI GEITA
WATAKIWA KUWEKA UTARATIBU MZURI KWA VIKUNDI KWENDA KUJIFUNZA UFUGAJI NYUKI
WILAYA YA BUKOMBE:
Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya Mkoani Geita wametakiwa
kuweka utaratibu mzuri wa vikundi vya wafuga nyuki kwenda kujifunza namna bora
ya ufugaji nyuki katika wilaya ya Bukombe ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa
katika zao la nyuki.
Akizungumza katika maadhimisho ya
siku ya utundikaji wa mizinga ya nyuki ambayo imefanyika kimkoa katika kijiji
cha Ikina wilaya ya Geita Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.Magalula Saidi ametoa wito
kwa wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya Mkoani hapa kuhakikisha kuwa
wanaweka utaratibu mzuri kwa vikundi vyote vya wafugaji wa nyuki kwenda wilaya
ya Bukombe ili wakaone namna wafugaji wa
nyuki wa huko walivyo piga hatua katika shughuli hiyo ili nao wanufaike.
“Natoa wito kwa wakurugenzi wote
kuweka utaratibu mzuri wa kuwapeleka wafugaji wa nyuki wilaya ya Bukombe ili
wakaone namna wenzao wanavyozalisha na kujipatia kipato na maendeleo kwa
kutumia fursa ya ufugaji nyuki kwani wilaya hiyo imewahi kutoa mshindi wa
kitaifa katika uzalishaji wa asali na ufugaji nyuki”.
Katika maadhimisho hayo Mkuu wa
Mkoa alikabidhi mizinga 50 ya nyuki kwa kikundi cha wafugaji nyuki cha Ikina
ambapo alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wanakijiji hao kwa jitihada hizo na
kuwataka kuendelea na moyo huo katika kujiletea maendeleo kupitia mradi wa
nyuki. Aidha Mhe. Mkuu wa Mkoa alimpongeza mzee Faustine Ntaliyo ambaye
alijitolea shamba lake la msitu wa asili lenye hekta 25 litumike katika
shughuli za kikundi hicho za ufugaji wa nyuki.
Halikadhalika Mhe. Mkuu wa Mkoa
aliwapongeza wakala wa huduma za misitu (TFS) kwa jitihada zao za kuwasaidia
wafugaji wa nyuki mizinga na kuzitaka taasisi zingine za umma na binafsi kutoa
misaada ya mizinga kwa vikundi mbalimbali vya wafugaji wa nyuki ndani ya Mkoa
wa Geita ili navyo vinufaike na miradi ya
nyuki.Aliwataka wananchi wote wa Mkoa wa Geita kuwekeza katika ufugaji
wa nyuki kwani hiyo ni fursa ya
kujiletea kipato na maendeleo katika kaya.
Katika maadhimisho hayo
Mhe.Magalula aliwataka maafisa biashara kuhakikisha kuwa wanatafuta masoko ya
uhakika ya asali na lakini pia maafisa nyuki wahakikishe wanatoa ushauri wa
kitaalam kwa wafugaji nyuki ili wazalishe kwa wingi na ubora.
Halmashauri ya wilaya ya Geita
imeahidi kuwa kukipatia kikundi hicho mabati ishirini 20 ambayo yatasaidia
kufunika mizinga ili kuiepusha kulowana kwa maji ya mvua kitendo ambacho
kitasaidia ubora wa asali pamoja na kutokuhama kwa nyuki.Hatahivyo kikundi
hicho kiliishukuru serikali kupitia wakala wa misitu kwa kuwapatia mizinga hiyo
50 ya kisasa yenye mifuniko iliyozibwa kwa juu na kuahidi kuitunza ili iweze
kuwapatia faida.
Mkoa wa Geita ni mmoja wa mikoa
ambao unazalisha asali yenye ubora wa hali ya juu hasa wilaya ya Bukombe ambayo
iliwahi kutoa mshindi wa kitaifa katika ufugaji wa nyuki.
Na: Magesa Jumapili (Geita)